nyarubamba

Wednesday, April 19, 2006

Siri za Mchuchuma, Liganga zafichuliwa

MIRADI ya Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa mbali ya kuwa na raslimali kubwa ya makaa ya mawe na madini ya chuma, pia una madini viambatanishi aina ya Titanium na Vanadium ambayo yana thamani kubwa hata kuliko dhahabu.

Siri hiyo imetolewa na Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Joseph Simbakalia, na kutoa tahadhari kwa serikali kuwa makini wakati wa kuchambua wawekezaji wanaokimbilia maeneo ya madini.

Alisema msukumo wa uzalendo kwa nchi yake unamsukuma zaidi kuhakikisha wawekezaji watakaopatikana kuendesha miradi ya umeme wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma, Liganga wawe waaminifu ili wananchi wafaidike na rasilimali zao.

Simbakalia, alisema wameamua kueleza kuwa Liganga ina chuma, lakini ukweli unaonyesha chuma hicho hubeba madini mengine yenye thamani zaidi.

Mradi wa mkaa wa mawe Mchuchuma na chuma, Liganga inahitaji Sh4.5 bilioni kwa ajili ya kukamilisha utafiti wa chuma. Utafiti wa Mchuchuma tayari umekamilika, kilichosalia ni kupatikana kwa mwekezaji, alisema.

Kulingana na utafiti wa awali unaonyesha asilimia 50 ni chuma, Titanium ni 12 na 0.5 ni Vanadium. Titanium hutumika kwenye viwanda vya kutengeneza rangi na vifaa vya plastiki na karatasi, ilhali Vanadium hutumika kutengeneza vifaa maalum vya chuma.

Kanali Simbakalia, alisema kwa bei ya mwaka jana ya chuma kwa tani ni dola 250 za Marekani, Titanium dola 2,500 na Vanadium ni maradufu ya bei ya dhahabu.

"Kutenganisha madini hayo yenye thamani kubwa na chuma, kunahitaji utaalam maalum, teknolojia sahihi na mtaji wa kutosha, lazima tulielewe hilo," alisema Simbakalia wakati akitoa maelezo kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara iliyotembelea miradi hiyo wiki iliyopita.

Kiwanda kitakachojengwa Liganga, kinatakiwa kiwe na uwezo wa kuzalisha tani 2.5 milioni, Titanium tani 250,000 na Vanadium tani 11,000 kwa mwaka. Kanali Simbakalia, alisema kikijengwa kiwanda hicho, kitakuwa ni kitovu cha viwanda mama katika eneo hilo.

"Kigezo ni uwezo wa mwekezaji basi...Mchuchuma inajitegemea, lakini Liganga inategemea Mchuchuma. Nenda dunia nzima kiwanda cha chuma kinategemea umeme wa mkaa wa mawe," alisema.

Aliongeza kuwa, Msumbiji inauza umeme Afrika Kusini inaozalisha kwa maji, lakini baada ya kuanzisha kiwanda cha chuma imeamua kununua umeme wa mkaa wa mawe kutoka Afrika Kusini na kwamba, nishati hiyo ndio inayotawala viwanda vya chuma dunia nzima.

"Tukipata fedha za utafiti wa Liganga, tunakuwa na uhakika wa nini tulichonacho. Lakini inatusaidia kuwa mradi kama huu tukishakuwa nao, tunajihakikishia kuwa tukitaka kuuza tunaongeza fedha kwenye akiba yetu," alisema mkurugenzi huyo na kuongeza:

"Suala la mwekezaji kuwa ataleta ajira ni upuuzi tu kwani, atakuja na wafanyakazi wote. Ajira ni kitu kidogo sana kwenye miradi kama hii." Alisisitiza kuwa mwekezaji katika eneo hilo lazima akubali kuwa atawajibika kwa uzalishaji wa madini hayo viambatanishi.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lilishafuta mradi wa Mchuchuma kwenye orodha ya miradi muhimu ya kutekelezwa kitaifa, bila kujali maamuzi ya serikali na gharama kubwa zilizobebwa juu ya maandalizi ya mradi huo.

Katika barua ya Tanesco ya Machi 29, 2005 inatamka wazi kuwa imefanya uamuzi mpya na sasa itazalisha umeme kwa kutumia gesi ya Songo Songo hadi itakapoisha, njia zingine ikiwemo Mchuchuma zitaangaliwa.

Hatua hiyo imelazimisha Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, kutoa maelekezo kwa serikali kwamba utekelezaji wa mradi huo sio wa hiari tena kwa sababu umeingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi.